Psalms 5

Sala Kwa Ajili Ya Ulinzi Wakati Wa Hatari

Kwa mwimbishaji. Kwa filimbi. Zaburi ya Daudi.

1 aEe Bwana, tegea sikio maneno yangu,
uangalie kupiga kite kwangu.
2 bSikiliza kilio changu ili unisaidie,
Mfalme wangu na Mungu wangu,
kwa maana kwako ninaomba.
3 cAsubuhi, unasikia sauti yangu, Ee Bwana;
asubuhi naleta haja zangu mbele zako,
na kusubiri kwa matumaini.

4 dWewe si Mungu unayefurahia uovu,
kwako mtu mwovu hataishi.
5 eWenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako,
unawachukia wote watendao mabaya.
6 fUnawaangamiza wasemao uongo.
Bwana huwachukia
wamwagao damu na wadanganyifu.

7 gLakini mimi, kwa rehema zako kuu,
nitakuja katika nyumba yako,
kwa unyenyekevu, nitasujudu
kuelekea Hekalu lako takatifu.
8 hNiongoze katika haki yako, Ee Bwana,
kwa sababu ya adui zangu,
nyoosha njia yako mbele yangu.

9 i jHakuna neno kinywani mwao linaloweza kuaminika,
mioyo yao imejaa maangamizi.
Koo lao ni kaburi lililo wazi,
kwa ndimi zao, wao hunena udanganyifu.
10 kUwatangaze kuwa wenye hatia, Ee Mungu!
Hila zao ziwe anguko lao wenyewe.
Wafukuzie mbali kwa sababu ya dhambi zao nyingi,
kwa kuwa wamekuasi wewe.

11 lLakini wote wakimbiliao kwako na wafurahi,
waimbe kwa shangwe daima.
Ueneze ulinzi wako juu yao,
ili wale wapendao jina lako
wapate kukushangilia.
12 mKwa hakika, Ee Bwana, unawabariki wenye haki,
unawazunguka kwa wema wako kama ngao.
Copyright information for SwhNEN